WANAFUZI watatu wa Shule ya Msingi Ussongo, kata ya Nyandekwa,
wilayani Igunga mkoani Tabora, wamepatiwa ujauzito. Wanamtuhumu mwalimu
wao, Baraka Samsoni.
Wanafunzi wanaodai wamepewa ujauzito na Mwalimu Samsoni,
ni  Christina Gordwin (15), Magdalena Bakari (15) na Lusia Maganga
(17). Wote watatu wanasoma darasa la saba shuleni hapo.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Christina ambaye hakuweza
kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi, alidai
kuwa  mahusiano ya kimapenzi na mwalimu wake yalianza tangu Januari
mwaka huu.
Naye Christina Mhindi (70) bibi wa Christina Gordwin amesema, siku ya
mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi alimpeleka mjukuu wake shuleni na
kuomba aruhusiwe kufanya mtihani lakini alikataliwa kutokana na kuwa na
ajauzito huo.
“Mjukuu wangu ameshindwa kufanya mtihani wake wa mwisho kwa sababu ya
ujauzito. Haingii akilini kuona walimu tuliowamini kufundisha watoto
wetu, ndiyo hao hao wanaowaharibu. Kinachoniuma zaidi, ni kuona hakuna
hatua zinazochukuliwa,”ameeleza.
Akiongea kwa uchungu huku chozi likimminika, Bi. Mhindi amesema,
“Kinachoniuma zaidi, mjukuu wangu anazuiwa kufanya mtihani, wakati
wenzake wawili waliopewa ujauzito na mwalimu huyo huyo, wameruhusiwa
kufanya mitihani yao.”
Falentina Lugamba, mwalimu mkuu wa shule hiyo, amekiri wanafunzi hao kupata ujauzito.
“Haya madai yapo ofisini kwangu. Nimeambiwa kuwa mwalimu Baraka ndiye
aliyewapa wanafuzi hawa ujauzito,” amesema Mwalimu Lugamba katika
mahojiano wiki hii.
Amesema kwa sasa mwalimu anayetuhumiwa kuwapa mimba wanafuzi
wake,  hayuko kazini na kuongeza, “Tayari nimetoa taarifa kwa ofisi wa
elimu wilaya kuhusu utoro wa mwalimu huyo.”
Kaimu ofisa Mtendaji wa kata ya Nyandekwa, Jaquiline Gube, amekiri
kupokea taarifa hizo kwa mmoja wa  wazazi wa  wanafunzi. Alisema
mzazi huyo ameomba kushughulikiwa; tayari amemwandikia mkuu wa shule na
mtendaji wa kijiji hicho kufuatilia suala hilo.
No comments:
Post a Comment